1 | GEN 1:1 | Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. |
2 | GEN 1:2 | Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji. |
3 | GEN 1:3 | Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. |
4 | GEN 1:4 | Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. |
5 | GEN 1:5 | Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza. |
6 | GEN 1:6 | Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” |
7 | GEN 1:7 | Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. |
8 | GEN 1:8 | Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili. |
9 | GEN 1:9 | Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. |
10 | GEN 1:10 | Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. |
11 | GEN 1:11 | Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. |
12 | GEN 1:12 | Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. |
13 | GEN 1:13 | Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu. |
15 | GEN 1:15 | nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. |
16 | GEN 1:16 | Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. |
18 | GEN 1:18 | itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. |
19 | GEN 1:19 | Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne. |
20 | GEN 1:20 | Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” |
21 | GEN 1:21 | Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. |
22 | GEN 1:22 | Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” |
23 | GEN 1:23 | Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano. |
24 | GEN 1:24 | Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. |
25 | GEN 1:25 | Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. |
26 | GEN 1:26 | Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.” |
27 | GEN 1:27 | Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba. |
28 | GEN 1:28 | Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.” |
29 | GEN 1:29 | Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. |
30 | GEN 1:30 | Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo. |
31 | GEN 1:31 | Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita. |
32 | GEN 2:1 | Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo. |
33 | GEN 2:2 | Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. |
34 | GEN 2:3 | Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya. |
35 | GEN 2:4 | Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa. Bwana Mungu alipoziumba mbingu na dunia, |
38 | GEN 2:7 | Bwana Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai. |
39 | GEN 2:8 | Basi Bwana Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. |
40 | GEN 2:9 | Bwana Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa kujua mema na mabaya. |
41 | GEN 2:10 | Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni, kuanzia hapa ukagawanyika kuwa mito minne. |
42 | GEN 2:11 | Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu. |
43 | GEN 2:12 | (Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri, bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.) |
44 | GEN 2:13 | Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi. |
45 | GEN 2:14 | Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki ya Ashuru. Mto wa nne ni Frati. |
46 | GEN 2:15 | Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. |
48 | GEN 2:17 | lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.” |
49 | GEN 2:18 | Bwana Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.” |
50 | GEN 2:19 | Basi Bwana Mungu alikuwa amefanyiza kutoka ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake. |
51 | GEN 2:20 | Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini. Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa. |
52 | GEN 2:21 | Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. |
53 | GEN 2:22 | Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume. |
54 | GEN 2:23 | Huyo mwanaume akasema, “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu na nyama ya nyama yangu, ataitwa ‘mwanamke,’ kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.” |
55 | GEN 2:24 | Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. |
56 | GEN 2:25 | Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu. |
57 | GEN 3:1 | Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?” |
59 | GEN 3:3 | lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ” |
60 | GEN 3:4 | Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. |
61 | GEN 3:5 | Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” |
62 | GEN 3:6 | Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala. |
63 | GEN 3:7 | Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika. |
64 | GEN 3:8 | Ndipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya Bwana Mungu alipokuwa akitembea bustanini jioni, wakajificha kutoka mbele za Bwana Mungu katikati ya miti ya bustani. |
66 | GEN 3:10 | Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.” |
68 | GEN 3:12 | Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami alinipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.” |
69 | GEN 3:13 | Ndipo Bwana Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.” |
70 | GEN 3:14 | Hivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili, “Umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa na wa porini! Utatambaa kwa tumbo lako na kula mavumbi siku zote za maisha yako. |
71 | GEN 3:15 | Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na wake, yeye atakuponda kichwa, nawe utamuuma kisigino.” |
72 | GEN 3:16 | Kwa mwanamke akasema, “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto. Tamaa yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala.” |
73 | GEN 3:17 | Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’ “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako, kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo siku zote za maisha yako. |
74 | GEN 3:18 | Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako, nawe utakula mimea ya shambani. |
75 | GEN 3:19 | Kwa jasho la uso wako utakula chakula chako hadi utakaporudi ardhini, kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo, kwa kuwa wewe u mavumbi na mavumbini wewe utarudi.” |
76 | GEN 3:20 | Adamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai. |
77 | GEN 3:21 | Bwana Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. |
78 | GEN 3:22 | Kisha Bwana Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyoosha mkono wake na kuchuma pia kutoka mti wa uzima akala, naye akaishi milele.” |
79 | GEN 3:23 | Hivyo Bwana Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa. |
80 | GEN 3:24 | Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki ya Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika huku na huko kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima. |
81 | GEN 4:1 | Adamu akakutana kimwili na mkewe Eva, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Eva akasema, “Kwa msaada wa Bwana nimemzaa mwanaume.” |
82 | GEN 4:2 | Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake. Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. |
83 | GEN 4:3 | Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa Bwana. |
84 | GEN 4:4 | Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, |
85 | GEN 4:5 | lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni. |
87 | GEN 4:7 | Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.” |
88 | GEN 4:8 | Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua. |
90 | GEN 4:10 | Bwana akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. |
91 | GEN 4:11 | Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. |
92 | GEN 4:12 | Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani asiye na utulivu.” |
93 | GEN 4:13 | Kaini akamwambia Bwana, “Adhabu yangu ni zaidi ya niwezavyo kustahimili. |
94 | GEN 4:14 | Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga asiyetulia duniani na yeyote anionaye ataniua.” |
95 | GEN 4:15 | Lakini Bwana akamwambia, “La sivyo, ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini atalipizwa kisasi mara saba zaidi.” Kisha Bwana akamwekea Kaini alama ili mtu yeyote ambaye angemwona asimuue. |
96 | GEN 4:16 | Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Bwana akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, iliyoko mashariki ya Edeni. |
97 | GEN 4:17 | Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Enoki. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Enoki jina la mtoto wake. |
98 | GEN 4:18 | Enoki akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli, Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, na Methushaeli akamzaa Lameki. |
99 | GEN 4:19 | Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila. |
100 | GEN 4:20 | Ada akamzaa Yabali ambaye ni baba wa wale walioishi katika mahema na kufuga wanyama. |
101 | GEN 4:21 | Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi. |
102 | GEN 4:22 | Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini. |
103 | GEN 4:23 | Lameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila nisikilizeni mimi; wake wa Lameki sikieni maneno yangu. Nimemuua mtu kwa kunijeruhi, kijana mdogo kwa kuniumiza. |
104 | GEN 4:24 | Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba, basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.” |
105 | GEN 4:25 | Adamu akakutana kimwili na mke wake tena, akamzaa mwana, akamwita Sethi, akisema, “Mungu amenijalia mwana mwingine badala ya Abeli, kwa kuwa Kaini alimuua.” |
106 | GEN 4:26 | Naye Sethi akamzaa mwana, akamwita Enoshi. Wakati huo watu wakaanza kuliitia jina la Bwana. |
107 | GEN 5:1 | Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu. Wakati Mungu alipomuumba Adamu, alimfanya kwa sura ya Mungu. |
108 | GEN 5:2 | Aliwaumba mwanaume na mwanamke, akawabariki. Walipokwisha kuumbwa, akawaita “mwanadamu.” |
109 | GEN 5:3 | Adamu alipokuwa ameishi miaka 130, alikuwa na mwana aliyekuwa na sura yake, mwenye kufanana naye. Akamwita Sethi. |
110 | GEN 5:4 | Baada ya Sethi kuzaliwa, Adamu aliishi miaka 800, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. |